Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Angelina Mabula ameisisitiza bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro na Uongozi wa chuo kuwa wabunifu na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ili waweze kujiendesha kama taasisi bila kusubiri kuhudumiwa na Serikali kuu.
Ametoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Chuo cha Ardhi Morogoro na kusisitiza kuwa chuo kinarasilimali nyingine endapo zitatumiwa ipasavyo zitakisaidia chuo kujisimamia kwa mujibu wa majukumu ya bodi.
Pia ameiagiza bodi hiyo kufuatilia na kurejesha mkopo wa kiasi cha shilingi Bilioni 1.2 ambao uliotolewa mwaka 2021 na serikali kwa lengo la kuisaidia Serikali kwenye zoezi la urasimishaji ambayo awali ilikuwa na changamoto kubwa na kudai kuwa urejeshaji wa Fedha hizo umekuwa wa kusuasua sana.
Mwenyekiti mpya wa bodi ya chuo hicho Balozi Job Masima amesema kuwa licha ya majukumu waliyonayo, bodi itaanza kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Waziri Mabula ili waweze kufanikisha lengo la serikali katika kuwahudumia wananchi hasa kwwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi.
Hata hivyo, Balozi Masima ameiomba mamlaka ya uteuzi kuwasaidia kumpata mkuu wa Chuo huku katibu tawala mkoa wa Morogoro Dkt. Musa Ally Musa akaomba uongozi wa chuo kuwapeleka wahitimu na Wanafunzi wanaohitaji kufanya mazoezi ya vitendo (field) kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ili wasaidiane katika kutatua changamoto za migogoro ya Ardhi.