Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna, Austria.
Kwa makubaliano hayo, Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna kitawajengea uwezo wataalamu wa mfumo wa mkojo, kugharamia utafiti na ubunifu pamoja na kufanya kambi ya pamoja ya matibabu na BMH.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dkt Alphonce Chandika, amesema makubaliano hayo yatawezesha wataalamu wa mfumo wa mkojo wa BMH kwenda Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna kuongeza ujuzi.
“Makubaliano haya yatasaidia kupunguza rufaa nje ya nchi kwa kuwezesha wataalamu wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna kuja Tanzania na kufanya kambi ya pamoja na wataalamu wetu,” alisema Dkt Chandika.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa na Dkt Chandika na Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna, Dkt Michaela Fritz yameshuhudiwa na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Austria, Bi Elizabeth Rwitunga.
Dkt Chandika na ujumbe wake wametembelea Idara ya Magonjwa ya Dharula (EMD).
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Vienna, Dkt Michaela Fritz, amesema makubaliano hayo yatasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wa mfumo wa mkojo wa BMH.
“Tumeingia makubaliano ya ushirikiano na Hospitali ya Benjamin Mkapa iliopo Tanzania ili kuwajengea uwezo katika eneo la mfumo wa mkojo,” alisema Dkt Fritz.