Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Ushindani nchini ( FCC) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bw. William Erio, walitembelea Bandari ya Tanga, tarehe 17 Februari, 2023 ili kujifunza masuala mbalimbali kuhusiana na utendaji kazi wa bandari hiyo.
Ziara hiyo ya mafunzo iliyokuwa sehemu ya ratiba ya shughuli za Baraza la Wafanyakazi la FCC, iliwawezesha watendaji hao kujifunza kwa vitendo utekelezaji wa majukumu ya uingizaji wa bidhaa nchini katika bandari hiyo na juhudi za Serikali za kupanua bandari hiyo ili kuiwezesha kuhudumia shehena nyingi zaidi za mizigo.
Msingi wa ziara hiyo ni FCC kuweza kujipanga zaidi katika kufanya kaguzi za bidhaa zinazoingia bandarini hapo ili kuhakikisha kuwa zinazingatia matakwa ya Sheria ya Alama za Bidhaa (1963), iliyorekebishwa, inayodhibiti na kuzuia uingizaji wa bidhaa bandia katika soko la Tanzania Bara.
Wajumbe hao wa FCC walipata fursa ya kutembelea maeneo ya bandari hiyo kama vile sehemu ya maegesho ya Meli (gati) na kufahamu kuhusu upanuzi wa bandari hiyo utakaoiwezesha kuhudumia ujazo wa tani 3,000,000 za mizigo kutoka tani 700, 000 za mizigo zinazohudumiwa hivi sasa, pindi upanuzi huo utakapokamilika ifikapo Mwezi Aprili, 2023.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FCC na Mkaguzi Mkuu wa Sheria ya Alama za bidhaa, Bw. Erio alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika katika kutekeleza miradi mikubwa inayowezesha ukuaji Jumuishi wa Uchumi wa Nchi na kuleta maendeleo kwa watanzania na huduma bora katika nchi jirani kupitia usafirishaji wa shehena zao kupitia miundombinu yetu.
Bw. Erio aliuhakikishia uongozi wa bandari hiyo kuwa FCC imejipanga kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kuendana na maboresho hayo.
“Tumeambiwa kuwa mara upanuzi huu utakapokamilika utaifanya bandari hii kuweza kupokea mizigo zaidi ya tani milioni 3 kwa mwaka kutoka tani laki 7 za sasa, hivyo FCC tuna wajibu wa kuisaidia Serikali na tutahakikisha tunajizatiti kutoa huduma zaidi za udhibiti wa bidhaa bandia bandarini hapa kwa weledi” alisema Bw. Erio.
Aliongeza kuwa katika kudhibiti bidhaa bandia kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Bidhaa (MMA), inayoisimamia, FCC itafanya kazi bega kwa bega na wadau wa kikosi kazi cha Kitaifa cha Udhibiti wa Bidhaa Bandia nchini sambamba na watendaji wa bandari hiyo ili kuhakikisha malengo ya Serikali kupitia bandari hiyo yanafanikiwa hivyo kuisaidia Serikali kutimiza malengo yake ya kukuza, kutoa huduma bora, kushamirisha biashara na kukuza uchumi nchini.
Alibainisha kuwa utendaji wenye weledi wa wadau wote katika utoaji huduma bora bandarini hapo, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa bidhaa bandia, zitawezesha mataifa yanayotumia huduma za bandari hiyo kunufaika na uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara kikanda na kimataifa, hususan sasa ambapo Bara la Afrika limeanzisha soko la pamoja la ACFTA.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa udhibiti wa bidhaa bandia nchini kutoka FCC, Bi. Khadija Juma Ngasongwa, alisema kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali, Kurugenzi ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia imejiimarisha kuhakikisha inadhibiti uingizaji wa bidhaa zote bandia katika maingilio ya bidhaa nchini, ikiwa ni pamoja na bandari hiyo.
Alisema ziara hiyo katika bandari ya Tanga itawawezesha kujipanga vyema zaidi katika kutekeleza majukumu ya udhibiti wa bidhaa bandia kwa madhumuni ya kushamirisha biashara kwa kulinda miliki bunifu na wakati huo huo kumlinda mtumiaji.