Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua Mpango Kabambe wa jiji la Mbeya 2019-2039.
Uzinduzi wa Mapngo huo umefanyika leo tarehe 21 Februari 2023 na kuhudhuruwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, madiwani , wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa taasisi za serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Dkt Mabula alisema lengo kuu la kuandaa mpango kabambe wa jiji la mbeya ni kutoa dira ya namna jiji la Mbeya litakavyopaswa kukua na kuendelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia 2019-2039.
‘’Mpango huu unaanisha mikakati ya uendelezaji na uboreshaji maeneo ya zamani yaliyojengwa kiholela kama vile sehemu za maeneo ya kata ya Sinde, Mahanga, Mabatini, Forest ya Zamani, Ilomba na Simike na maeneo kongwe yaliyochakaa sana’’ alisema Dkt Mabula.
Mpango Kabambe uliozinduliwa umetaja mikakati minne ya kusimamia ukuaji na maendelezo ya jiji la Mbeya ambayo ni uendelezaji upya maeneo kongwe, kurasimisha makazi ambayo kimipangomiji hayajaathirika sana lakini kuna uwezekano wa kupata miundombinu, kusimamia yasiyoathirika kwa kuvamiwa na ujenzi holela pamoja na mkakati wa kuanzisha miji ya pembezoni.
Dkt Mabula ametoa wito kwa taasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwenye jiji la Mbeya kuutumia Mpango Kabambe ulioandaliwa katika utekelezaji wa shughuli zao na miradi mbalimbali ya maendeleo.