Mwalimu katika shule ya sekondari ya binafsi katika mji wa Ufaransa wa Saint-Jean-de-Luz karibu na Biarritz ameuawa kwa kuchomwa kisu na mwanafunzi siku ya Jumatano alipokuwa akifundisha darasani.
Mshukiwa wa shambulio hilo, mwenye umri wa miaka 16, alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi na mwathiriwa alikuwa mwalimu wa Kihispania mwenye umri miaka 56.
“Ninaweza kuthibitisha kwamba kumekuwa na kuchomwa kisu na kwamba mwathiriwa amekufa”
mwendesha mashtaka wa umma huko Bayonne, Jerome Bourrier, aliiambia shirika la AFP.
Matukio hayo yalifanyika katika shule ya Kikatoliki ya Saint-Thomas d’Aquin huko Saint-Jean-de-Luz, yapata kilomita 20 kusini mwa Biarritz karibu na mpaka wa Uhispania.
Hii ni mara ya kwanza kwa mwalimu kuuawa wakati wa majukumu yake nchini Ufaransa tangu mauaji ya Samuel Paty katika msimu wa vuli mwaka 2020.