Wanafunzi wanne wa Shule ya misingi Kagera iliyopo Manispaa ya Kigoma ujiji Mkoani Kigoma wanasadikiwa kufariki baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvuka katika Mto Luiche kuelekea Shuleni kuzama.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Kigoma Inspekta Jacob Chacha amethitibisha kutokea kwa tukio hilo majira ya saa moja na nusu asubuhi ambapo licha ya kufanya msako wa uokozi lakini bado miili ya Wanafunzi hao haijapatikana.
Tangu majira ya saa moja na nusu asubuhi ya leo wakati tukio hilo linatokea mpaka hivi sasa licha jitihada za uokozi kufanywa na Askari wa Zimamoto na Uokoaji bado miili hiyo haijaonekana kwani Mto huo hupeleka maji yake katika Ziwa Tanganyika.
Wananchi wameeleza matukio ya vifo ya Watu kutokana na kuzama katika Mto huo ni mengi lakini hili la Wanafunzi akiwemo wa umri wa miaka 6 na 8 limekuwa na hisia kali hata zaidi na majonzi wa Wananchi.
Wanafunzi ambao hadi sasa hawajulikani walipo ni Ashura Haruna darasa la kwanza, Zabibu Jumanne darasa la pili (8), Ramadhani Kwila darasa la tano (12) na Tatu Sanaari darasa la kwanza (6) huku ambao wameokolewa wakiwa ni Issa Omary darasa la 6 na Michael Logoro darasa la kwanza.