Ni kipindi cha katikati ya wiki hii ambapo tulianza kusikia kuhusu kikundi kinaitwa Panya road ambapo kwa wakazi wa maeneo ya kigogo mpaka Mburahati na maeneo mengine kama Ilala na Buguruni wamelalamika juu ya vijana hao ambao wanajikusanya na kutembea pamoja wakiwa zaidi ya 30 na endapo ukikutana nao watachukua pesa au simu za mkononi au kingine chochote.
Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam May 24 2014 limefanya kikao cha makamanda wote wa jiji hili kisha baadae kuitwa waandishi wa habari.
Makundi hayo ni pamoja na vijana wahuni wasio na kazi maalum maarufu kwa jina la MBWA MWITU au PANYA ROAD ambapo maeneo yote yaliyotajwa kuonekana vijana hao ni pamoja na Kigogo, Magomeni, Tabata, Manzese na maeneo ya Mbagal.
Sasa hivi wamepangwa askari wa kutosha wa doria ili kudhibiti mlipuko wowote wa vitendo vya kihuni vyenye ishara ya uhalifu vinavyoleta hofu kwa wananchi.
Kwa ujumla ni kwamba vijana hao hawana uwezo tena wa kufanya uhalifu katika makundi yao kutokana na mpango kazi uliopangwa na jeshi la Polisi Kanda maalum na kwa sasa tayari wamashakamatwa viongozi [Ring Leaders] sita wa vikundi hivyo na majina yao ni haya
- ATHUMAN SAID Miaka 20 Mkazi wa Kigogo.
- JOSEPH PONELA Dereva Bodaboda,Mkazi wa Kigogo Mkwajuni.
- CLEMENT PETER Miaka 25,Fundi Seremala,Mkazi wa Kigogo.
- ROMAN VITUS Miaka 18,Mfanya biashara Mkazi wa Kigogo.
- MWINSHEHE ADAM Miaka 37, Mkazi wa Temeke Mashine ya Maji.
- DANIEL PETER Miaka 25,Mkazi wa Yombo.
Pamoja na udhibiti wa vijana hao, unaambiwa umezuka mtindo wa watu ambao hawafahamiki maeneo mbalambali ya jiji la Dar es salaam kutuma ‘sms’ wakieneza uvumi kwamba maeneo yao yamevamiwa na makundi Mbwa Mwitu au Panya Road ukiwa ni mtindo ambao umeenea sanaKigogo,Magomeni,Manzese na Tabata.
Kufuatia hilo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kuwa mtindo huo uishe kwa sababu wanasababisha hofu kwa wananchi bila sababu na Jeshi la polisi limebaini kuwa hakuna tukio lolote ambalo limefanyika maeneo hayo au kuripotiwa kituo chochote cha Polisi katika kipindi cha wiki hii ambapo uvumi ulienea sana.
Jeshi la polisi limewatoa hofu wananchi wa Dar es Salaam kwamba si kweli kuna tishio la vijana hao kama inavyosemekana kwani jeshi la Polisi limejiimarisha kiulinzi na vijana hao hawana uwezo wa kufanya watakavyo kama uvumi ulivyoenezwa kimakosa.
Uchunguzi umebaini kwamba chanzo cha uvumi huo ni tarehe 18/05/2014 na 20/05/2014 kulitokea mauaji ya vibaka wawili waliohusishwa na makundi haya na kwamba kulikuwa na hofu kuwa baada ya mazishi vijana wenzao wangeweza kulipiza kisasi ndio maana pakawa na uvumi wa jumbe mbalimbali zilizoleta hofu.