Wakulima wa Kijiji cha Ulemo kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani Singida wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbolea ya ruzuku ambapo sasa wameanza kuona matokeo yake.
Wananchi hao wamebainisha hayo leo Machi Mosi, 2023 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wilayani humo ambapo ameshiriki mkutano wa shina namba 6 katika Kijiji cha Ulemo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mjumbe wa mkutano huo, Peter Paulo ameishukuru Serikali kwa kuwafikishia mbolea hiyo kwa bei nafuu tofauti na waligokuwa wakinunua siku za nyuma.
“Tunashukuru kwa kutuletea mbolea ya ruzuku, tunaitumia vizuri na tunatarajia kupata mavuno mazuri msimu huu,” amesema mjumbe huyo wakati akijadili ajenda ya Maendeleo katika shina lake.
Kwa upande wake, Happiness Kitundu amesema ameipongeza serikali kwa kuwaletea maendeleo hasa suala la mbolea ya ruzuku huku akiomba wajengewe kituo cha afya katika kata yao.
“Katika kijiji chetu (Ulemo) tuna Zahanati lakini tunaomba tujengewe kituo cha afya kwa sababu kuna ajali huwa zinatokea katika Mlima Sekenke, hivyo itakuwa ni rahisi kupata matibabu hapa hapa,” amesema.
Kwa upande wake, Chongolo amewapongeza kwa kuchapa kazi na kwamba Serikali ya CCM imetoa ruzuku ili kuwapunguzia bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea ambayo ilikuwa bei juu.
“Wote mnajua kabla ya mbolea bei ilikuwaje, lakini sasa baada ya serikali kutoa ruzuku, bei imeshuka na wakulima mnapata mbolea kwa nafuu,” amesema Chongolo wakati akizungumza na wananchi hao wa Ulemo.