Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema dunia haijachukua hatua za maana kulinda haki za wanawake, na kwamba usawa wa jinsia katika kona zote za dunia inaonekana ajenda ambayo ipo karne nyingi nyuma kufikiwa.
Antonio Guterres alisema hayo jana Jumatatu katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, harakati za kupigania haki za wanawake zimefifia kwa kiwango cha kutisha hasa katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita.
Amesema kwa mujiibu wa viwango vya Taasisi ya Usawa wa Jinsia na Kumuwezesha Mwanamke, dunia ipo miaka 300 nyuma kufikia usawa unaorodhisha baina ya wanaume na wanawake katika masuala mbalimbali.
Guterres amezitolea mwito serikali za dunia, asasi zisizo za kiraia na sekta binafsi kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba kunakuwepo na usawa wa kijinsia katika nchi zote duniani.
Guterres ameeleza bayana kuwa, jamii nyingi duniani zinabaki nyuma kimaendeleo katika maeneo ambayo kunakuweko na pengo kubwa la usawa wa kijinsia.
Amesema kukosekana usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika nchi tofauti husababisha hasara ya mamilioni ya dola kwa sekta ya uchumi katika maeneo mbalimbali duniani.