Ripoti iliyotolewa jana Jumanne na UNICEF imeeleza kuwa, nchi 12 zenye viwango vya kutisha vya umaskini zimesajili ongezeko la asilimia 25 ya kesi za utapiamlo miongoni mwa wanawake wajawazito katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Nchi hizo 12 zilizosajili ongezeko hilo la kuogofya kutokana na kupanda kwa bei ya chakula na migogoro tofauti ni pamoja na Afghanistan, Burkina Faso, Chad, Ethiopia, Kenya, Mali, Niger, Nigeria, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Yemen.
UNICEF imesema idadi ya wajawazito na wanawake wanaonyonyesha wakiwemo wasichana waliobalehe wanaosumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu imeongezeka kutoka milioni 5.5 mwaka 2020, hadi milioni 6.9 mwaka jana 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Catherine Russell ameonya kuwa, baa la njaa limesababisha mamilioni ya wanawake na watoto wao kutumbukia katika dimbwi la njaa na utapiamlo wa kiwango cha juu.
Takwimu za Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa FAO zinaonesha kuwa, watu takriban milioni 239 wa Afrika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara wanakabiliwa na tatizo la njaa na utapiamlo.
Ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura na makusudi kunusuru maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana wenye mimba na wanaonyonyesha. UNICEF ilitoa takwimu hizo mpya za kutamausha jana Jumanne, siku moja kabla ya dunia kuadhimisha hii leo Siku ya Kimataifa ya Wanawake.
Chanzo: aljazeera.