Watu wanane Wakazi wa Kijiji cha Ipalamasa Mkoani Geita wamefariki Dunia kwa kufukiwa na kifusi wakati walipokuwa wakifanya shughuli za uchimbaji madini katika eneo lililozuiliwa na Serikali kufanya shughuli hizo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema Watu hao walivamia katika eneo ambalo tayari lilizuiliwa na Serikali na limekuwa likilindwa lengo likiwa kutohatarisha maisha ya Wachimbaji.
“Ni kweli lipo hili tukio la Watu ambao walivamia eneo la Mgodi ambao haujawa rasmi kufanya uchimbaji hatimaye kusababisha maafa na hadi sasa hivi Wananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wameipata miili ya Watu wanane wakiwa wameshafariki Dunia”
Kamanda Jongo amesema matukio kama hayo ya Wachimbaji kufukiwa na vifusi yamekuwa yakitokea mara kwa mara huku akiwataka Wananchi pamoja na Viongozi wa Serikali ngazi ya Mtaa kuhakikisha wanashirikiana katika kulinda maeneo ambayo tayari yamepigwa marufuku kufanya shughuli hizo”