Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amewapongeza familia ya Mama Amne Salim, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Dk.Salim Ahmed Salim kwa kutoa mchango wao katika kuendeleza tafiti nchini na kuelekeza ufadhili wao, ili kuisaidia Serikali na Wananchi wa Tanzania kulielewa janga la Ugonjwa wa Uviko-19.
Aliyasema hayo alipofungua Kongamano la kusambaza Matokeo ya tafiti za Uviko-19, zilizofanywa na Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS) kupitia mfumo wa ufadhili wa Mama Amne Salim uliyofanyika jengo la CHPE kampasi ya Muhimbili Dar es salaam tarehe 21 Machi, 2023.
Aidha, Rais Dk.Mwinyi amesema taifa bora hujengwa na raia wenye afya pia kupitia tafiti zinazofanyika hapa nchini kwa kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu changamoto zinazotukabili katika sekta ya afya Serikali upande wa Tanzania bara na Zanzibar ziko tayari kutumia matokeo ya tafiti hizo kwa maslahi ya Taifa.
Pia amepata faraja kusikia Chuo cha MUHAS kimekuwa cha kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kati , kutokana na tafiti , machapisho wanayofanya pia amewaasa kazi zao ziweze kuleta unafuu kwa wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili katika malengo endelevu.
Vilevile, alieleza ushirikiano uliopo kati ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na MUHAS katika kutayarisha mitaala, kusomesha walimu na wataalamu wa afya kwa kuendelea kuimarisha Shule kuu za tiba na afya ya kinywa. Pia amewashukuru kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kazi yao katika kuishauri Wizara ya Afya Zanzibar kwa kuunda miongozo mbalimbali kusaidia maboresho sekta ya Afya Zanzibar.