Paul Rusesabagina, aliyepata umaarufu baada ya kuokoa Maelfu ya Watu katika mauaji ya kimbari Rwanda akiwa Meneja wa Hoteli na baadaye ujasiri wake uliigizwa kama Shujaa kwenye Filamu ya Hollywood kuhusu vita vya Rwanda inayoitwa Hotel Rwanda, ataachiwa huru leo Jumamosi.
DW Kiswahili wameripoti kuwa Rusesabagina ambaye anatumikia kifungo cha miaka 25 jela nchini Rwanda baada ya kushtakiwa kwa makosa ya kuhusika na ugaidi alihukumiwa September mwaka 2021 baada ya kukutwa na hatia ya kuwa na mahusiano na mtandao unaoupinga utawala wa Rais Paul Kagame.
Kwa mujibu wa chanzo cha Serikali ya Rwanda, Rusesabagina kwanza atasafirishwa kwenda Doha na baadaye kupelekwa nchini Marekani, hatua ya kuachiwa kwake imekuja baada ya Shujaa huyo wa Hotel Rwanda kumuandikia barua Rais Paul Kagame kuomba ahurumiwe.
Marekani imekuwa ikisema Rusesabagina anazuiliwa kimakosa kwasababu ya kile ilichosema ni kukosekana haki katika undeshaji wa kesi, Rusesabagina ni Raia wa Rwanda mwenye ukaazi wa kudumu wa Marekani.