Kiongozi wa Kanisa katoliki Papa Francis alilazwa hospitali Jumatano kutokana na maambukizi ya mapafu baada ya kukabiliwa na matatizo ya kupumua katika siku za hivi karibuni, na atakaa hospitali kwa siku kadhaa za matibabu, Vatican ilisema.
Msemaji wa Vatican Matteo Bruni amesema katika taarifa kwamba Papa mwenye umri wa miaka 86 hana Covid 19.
Hii ni mara ya kwanza kwa Francis kulazwa hospitali tangu alipokaa siku 10 katika hospitali ya Gemelli mwezi Julai mwaka wa 2021 na kufanyiwa upasuaji kwenye matumbo.
Maswali yameibuka kuhusu hali ya afya ya Francis na uwezo wake kusherekea matukio mengi ya wiki takatifu ambayo inaanza mwishoni mwa wiki hii na Jumapili ya matawi.
Maaskofu katika makanisa kote Italia wanamuombea Francis apone haraka, Urais wa Baraza la Maaskofu wa Italia, kwa niaba ya maaskofu wa Italia, ulisema katika taarifa siku ya Jumatano.
“Katika kumtakia Baba Mtakatifu apone haraka, Ofisi ya Rais inamkabidhi Bwana madaktari na wahudumu wa afya ambao kwa taaluma na kujitolea wanamhudumia yeye na wagonjwa wote,” iliongeza.