Msemaji wa Serikali ya Burkina Faso amesema wanahabari hao wamefukuzwa nchini humo kwa kuandika habari na makala za uwongo na upotoshaji ili kuichafua sura ya nchi.
Maripota hao waliwasili Paris jana Jumapili, baada ya kutimuliwa nchini Burkina Faso juzi Jumamosi.
Uongozi wa gazeti la Kifaransa la Le Monde umesema katika taarifa kuwa: Ripota wetu nchini Burkina Faso, Sophie Douce amefukuzwa nchini humo, sawa na mwenzake wa gazeti la Libération, Agnes Faivre.
Toleo la Machi 27 la gazeti la ‘Libération’ lilichapisha habari ya upekuzi, iliyoonesha mauaji yaliyofanywa na eti na askari wa nchi hiyo, dhidi ya watoto na vijana mabarobaro katika kambi za kijeshi nchini humo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Burkina Faso ilisimamisha matangazo ya kanali ya televisheni ya Ufaransa ya France 24, baada ya chombo hicho kurusha hewani mahojiano kiliyoyafanya na kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda tawi la Kaskazini mwa Afrika AQIM.
Jean-Emmanuel Ouedraogo, Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso alisema katika taarifa kuwa, “France 24 si tu imegeuka na kuwa msemaji wa hawa magaidi, lakini mbaya zaidi, imekuwa uwanja wa kuhalalisha vitendo vya kigaidi na matamshi ya chuki.”
Huu ukiwa ni muendelezo wa hatua za nchi hiyo Afrika Magharibi za kukabiliana na vyombo vya habari vya nchi hiyo ya Ulaya.