Kwa mujibu wa jarida la Forbes, utafiti wa hivi karibuni wa Idara ya Lishe na Fiziolojia katika Chuo Kikuu cha Utah nchini Marekani unaonyesha kuwa kufunga mara kwa mara kunaweza kukusaidia kuishi maisha marefu.
Watu wanaofunga na kuacha kula kwa noba na mara kwa mara hula chakula kwa wakati maalumu. Utafiti unaonyesha kuwa kufunga na kuacha kula kwa idadi fulani ya masaa kwa siku au kula mlo mmoja tu kwa siku kadhaa kwa wiki kunaweza kuwa na faida za kiafya.
Kufunga na kuacha kula katika nyakati makhsusi za siku kunatofautiana kikamilifu na aina zingine za lishe na mpangilio maalumu wa ulajii chakula (diet) kwa sababu sio lazima kubadilisha kile unachokula ili kupata matokeo mazuri. Hata hivyo, hii haina maana kwamba unaweza kula lishe mbaya na chakula chenye kalori nyingi.
Wataalamu wanapendekeza kula vyakula mbalimbali vyenye virutubisho muhimu ambavyo vitakusaidia kujisikia vizuri hata wakati wa mfungo.
Kufunga katika vipindi maalumu kunaweza pia kusaidia kulinda viungo mbalimbali vya mwili mkabala wa magonjwa. Ushahidi mwingi unaonyesha kuwa, kudumisha mpangilio wa mlo huo (diet) kunaweza kuzuia na hata kukomesha baadhi ya magonjwa sugu, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, kisukari aina ya 2, na matatizo ya neva yanayohusiana na umri.