Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI imetangaza kuwa, imemtia mbaroni mvujishaji wa nyaraka za siri za kiintelijensia za jeshi la nchi hiyo.
Hivi karibuni, nyaraka za siri na maelezo ya mpango wa Marekani na NATO wa kulizatiti kwa silaha na zana za kivita jeshi la Ukraine kwa ajili ya kuishambulia kijeshi Russia, pamoja na nyaraka nyingine za siri za utawala wa Biden, zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya Twitter na Telegram, na hivyo kuibua hisia na tafukari nyingi kutokana na kufichuliwa na kuwekwa hadharani matukio mengi katika nyanja mbalimbali.
Maafisa wa Marekani katika ngazi tofauti wangali wanahangaika kudhibiti athari hasi za ndani na nje ya nchi zinazotokana na uvujishaji wa nyaraka hizo 100 za siri na za siri kubwa katika mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran IRNA, FBI ilitangaza katika taarifa jana Alhamisi kwamba imemkamata mshukiwa wa uvujishaji wa nyaraka za taarifa za siri kubwa katika mitandao ya kijamii na ingali inaendelea kufanya uchunguzi katika makazi ya mtu huyo.
FBI ilisema imemkamata mtu mmoja na inaendelea na taratibu za kisheria katika makazi ya mtu huyo huko North Dutton, jimboni Massachusetts.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu Merrick Garland mtu huyo amekamatwa kuhusiana na uchunguzi wa madai ya uondoaji, uhifadhi na usambazaji bila kibali wa taarifa za siri za masuala ya ulinzi wa taifa.
Hapo awali, maafisa wa Marekani walitangaza kuwa mshukiwa huyo anaitwa Jack Teixeira.
Gazeti la New York Times, ambalo ndilo lililofichua jina lake kwa mara ya kwanza, liliripoti kwamba Teixeira mwenye umri wa miaka 21 ni askari wa kikosi cha taifa cha ulinzi katika jimbo la Massachusetts na kijana huyo ni askari wa tawi la jasusi la walinzi wa taifa.