Polisi ya Iran ilitangaza kuanza kutumika kwa hatua mpya za kudhibiti uvaaji wa hijab kuanzia Jumamosi Aprili 15 na kuwalazimisha wanawake kuheshimu uvaaji wa hijabu nchini Iran tangu mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979. Jumapili hii, polisi wamepitisha hatua kutekeleza uvaaji wa sitara ya Kiislamu.
Kulingana na msemaji wa polisi, jumbe 3,500 za onyo zilitumwa kwenye migahawa au vituo vya ununuzi kwa kutoheshimu uvaaji wa hijabu na 137 kati yazo zilifungwa kote nchini kwa kurudia kosa hilo.
Polisi ilitangaza kwamba kamera mpya za uchunguzi zitafanya iwezekane kutambua kwenye barabara, kwenye magari au katika vituo vya ununuzi, wanawake ambao hawaheshimu uvaaji wa hijabu ,maonyo ya SMS pia yalitumwa kwa wanawake ambao hawavai sitara ya Kiislamu na, ikitokea kurudi kosa, watafikishwa mbele ya mahakama. Watalazimika kulipa faini na watanyimwa baadhi ya huduma za kijamii na wanaweza kuzuiwa kuondoka nchini.
Magari yanayoendeshwa na wanawake ambao hawajavaa hijabu yanaweza kukamatwa kwa wiki kadhaa zinazokuja.
Tangu kifo cha Mahsa Amini mwezi Septemba, aliyekamatwa na polisi wa maadili kwa kutoheshimu uvaaji wa hijabu, idadi ya wanawake wasiovaa hijabu mitaani imeongezeka kama ishara ya kupinga.
Hatimaye naibu mwendesha mashtaka nchini humo ametangaza kuwa wale wanaowahimiza wanawake kutovaa hijabu wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka kumi jela.
Wanawake nchini Iran bado watahitajika kuvaa hijabu chini ya sheria ya Jamhuri ya Kiislamu, hata kama serikali ya nchi hiyo itaamua kuwafuta polisi wa kidini waliokuwa na jukumu la kutekeleza kanuni za mavazi.
Mwanasheria Mkuu wa Iran Mohammad Jafar Montazeri alitangaza Jumamosi kuwa polisi wa maadili ya nchi hiyo wamevunjwa, na kuongeza kuwa mfumo wa mahakama utaendelea kufuatilia mienendo ya watu nchini humo.
Takriban watu 448, wakiwemo watoto 60, wameuawa tangu maandamano hayo yaanze, ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kwa sababu ya ugumu wa kupata vyeti vya kifo, kulingana na NGO ya Iran ya Haki za Kibinadamu.