Mahakama moja mjini Malindi Pwani ya Kenya imewaruhusu polisi nchini humo kumzuilia mhubiri mwenye utata Paul Nthenge Makenzi kwa siku 14 zaidi ili kuruhusu maafisa wa upelelezi kukamilisha uchunguzi kuhusu shughuli zinazodaiwa kuwa za mhubiri huyo zinazoaminika kusababisha vifo vya wafuasi wake sita ambao wakiwa wamefunga kula chakula wakiwa na matumaini ya kumuona Yesu Kristo kufuatia maagizo yake.
Mhubiri huyo wa kanisa la Good News International amezuiliwa pamoja na wafuasi wake wengine sita mpaka sasa.
Akitoa uamuzi huo, hakimu mkuu wa mahakama ya Malindi, Elizabeth Usui alitupia mbali dhamana ya shilingi elfu 10 aliyopewa Mackenzie katika kesi ya awali ambapo mhubiri huyo alishukiwa kuhusika katika vifo vya watoto wawili kupitia ushawishi wake.
Familia ya baadhi ya wafuasi hao wamefika eneo hilo wengi wao wakitoka maeneo ya Kisumu, Kapsabet, Kajiado Machakos na hata kaunti ya Kilifi.
Siku ya alhamis watu wanne walipatikana wakiwa wamefariki na wengine zaidi ya kumi walilazwa hospitalini katika huko Kilifi nchini Kenya, baada ya kuokolewa wakisubiri mwisho wa dunia unaokaribia.
Polisi walisema kundi hilo lilipatikana katika msitu walimokuwa wakiishi kwa siku kadhaa baada ya kuambiwa na mhubiri wa eneo hilo kufunga huku “wakingoja kukutana na Yesu” na mamlaka ilisema iliokoa watu 11 – sita kati yao walikuwa wamedhoofika na katika hali mbaya ya afya.
Inasemekana waumini hao wa kanisa la Good News International Church linaloongozwa na mchungaji wa eneo hilo ambaye anashikiliwa na jeshi la polisi alidaiwa kuwataka waumini wake kufa njaa ili kufika mbinguni kwa kasi.