Waendesha mashtaka wa Marekani wamewakamata wanaume wawili mjini New York kwa madai ya kuendesha “kituo cha polisi cha siri” cha China katika kitongoji cha Chinatown cha Manhattan.
Lu Jianwang mwenye umri wa miaka 61 na Chen Jinping ana miaka 59, wote wakazi wa Jiji la New York, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kuwa mawakala wa China na kuingilia mfumo wa haki na wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya shirikisho huko Brooklyn siku ya Jumatatu.
Vituo hivyo vya polisi vinaaminika kuwa takribani 100 vinavyofanya kazi duniani kote katika nchi 53, ikiwemo Uingereza na Uholanzi na mwezi uliopita, polisi wa shirikisho la Canada walitangaza uchunguzi katika maeneo mawili ya eneo la Montreal yanayofikiriwa kuwa vituo vya polisi vya siri vya China.
Bw Lu wa Bronx na Bw Chen wa Manhattan walifanya kazi pamoja kuanzisha kituo cha kwanza cha polisi wa nje ya nchi, nchini Marekani kwa niaba ya Wizara ya Usalama wa Umma ya China, Idara ya Sheria ya Marekani ilitoa madai hayo siku ya Jumatatu.
Kituo hicho kilifungwa mnamo mwaka 2022, idara hiyo ilisema, baada ya waliohusika kufahamu uchunguzi wa FBI katika kituo hicho.
“Mashtaka haya yanafichua ukiukaji wa wazi wa serikali ya China kwa kuanzisha kituo cha polisi cha siri katikati ya Jiji la New York,” Breon Pearce, mwendesha mashtaka mkuu huko Brooklyn alisema.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, Bw Lu alikuwa na uhusiano wa karibu na watekelezaji sheria wa China, na aliorodheshwa kuisaidia China na shughuli za ukandamizaji nchini Marekani kuanzia mwaka wa 2015, ikiwa ni pamoja na kuwanyanyasa wapinzani wa China.
Mnamo mwaka 2018, alidaiwa kushiriki katika juhudi za kushinikiza mkimbizi wa China kurudi China, ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa mara kwa mara na vitisho kwa mtu huyo na familia yake, wanaoishi China na Marekani.
Awali China ilikanusha kuendesha vituo hivyo, na kuviita vituo vya huduma kwa raia wa ng’ambo.
Washukiwa hao walihojiwa na mamlaka mnamo Oktoba 2022, wakati FBI ilipofanya msako katika kituo kilichoshukiwa. Simu zao zilinaswa kama sehemu ya msako huo na wote wawili walikiri kuwa walifuta mawasiliano na afisa wa Wizara ya Usalama wa Umma wa China ambaye anadaiwa kuwasimamia nchini Marekani, waendesha mashtaka walidai.
Iwapo watapatikana na hatia, Bw Lu na Bw Chen wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 jela.