Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida amependekeza kupandishwa hadhi kwa Chuo cha Kilimo Uyole jijini Mbeya ili kitoe mafunzo ya shahada.
Kwa sasa, Chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 400 kinatoa mafunzo ya kilimo na mifugo kwa ngazi ya astashahada na stashahada pekee.
Kawaida alitoa kauli hiyo jana, alipotembelea vijana walionufaika na mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), wanaopata mafunzo chuoni hapo, ikiwa ni ziara yake ya kutembelea mradi huo katika Mikoa ya Dodoma, Mbeya, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Mtwara.
Pendekezo lake hilo, linatokana na kile alichoeleza kuwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo inayoongoza kwa shughuli za kilimo.
“Hatutakuwa tunatenda haki kama Chuo hiki kilichopo katika Mikoa inayolisha Tanzania, kiishie kutoa mafunzo kwa ngazi za chini, tunataka kipande hadhi,” alisema.
Katika kulitekeleza hilo, alisema mamlaka zinazohusika zikae chini kuchakata taratibu na kama inawezekana ziweke bayana.
Kuhusu mradi wa BBT, Kawaida alitaka juhudi ziongezwe kuhakikisha idadi ya wanaodahiliwa kila muhula inaongezeka ikilinganishwa na ya sasa.
Kauli yake hiyo inatoka na kile alichofafanua kuwa, idadi ya waliodahiliwa kwa muhula wa kwanza wa mradi huo unaohusisha miezi minne ni vijana 812 kati ya takriban 20,000 walioomba.
Kwa mujibu wa Kawaida, iwapo katika kila muhula wa miezi minne watakaochaguliwa ni 812, hadi kufikia mwaka 2030 mwisho wa mradi ni vijana 22,736 pekee ndiyo watakaokuwa wamenufaika ambao ni chini ya makusudio.
“Tunalenga kuwanufaisha vijana 200,000 lakini kwa idadi hii ya tunaodahili kwa muhula kuna haja ya kuongeza mbinu ili kwa muhula wadahiliwe wengi zaidi na tufikie lengo,” alisema.