Mkuu wa wilaya ya Morogoro Rebecca Nsemwa amekerwa na kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi shuleni ambapo amewataka wazazi kuanza mara moja kuchanga chakula ili wanafunzi waanze kupata chakula shuleni.
DC Nsemwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Juma la Elimu Tanzania uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mvuha katika Kata ya Mvuha Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini, ambapo Juma la Elimu hufanyika kila Mwaka kwa kuandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Elimu na Serikali.
Anasema wazazi wamekua chanzo cha wanafunzi kushuka ufaulu kwa kukataa kuchangia chakula na kwamba ili wanafunzi wafaulu lazima wapate chakula waweze kuelewa masomo ya darasani hivyo ni lazima wazazi kuanza kuchangia chakula na michango hiyo ipitie kamati za shule zao na sio kwa walimu.
“mnawapa wakati mgumu walimu wetu kufundisha watoto wenye njaa hawaelewi ,chakula wanachokula nyumbani ndo hichohicho watakula shuleni”
Nsemwa anasema hata utoro kwa wanafunzi unaweza kupungua endapo watakua wanapata chakula shuleni kwani wanafunzi wengine wana umri mdogo wanahitaji kula chakula ili mwili uweze kufanya kazi
Kwa upande wake mratibu wa maadhimisho ya Juma la Elimu kitaifa, ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Ochola Wayoga amesema lengo la kuanda maadhimisho hayo ni kuongeza chachu ya ufaulu kwa wanafunzi hasa vijijini.
Ochola wayoga amesema maadhimisho hayo yanasaidia watoto kubadilisha uwezo na kufahamu vitu vingi kutoka kwa wanafunzi wengine kwa kuona teknolojia na ubunifu.
Naye moja wa walimu Paschal Martine ametoa wito kwa wazazi kusomesha watoto badala ya kuwakatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuolewa na shughuli za kilimo
Anasema serikali inajenga madarasa mengi katika wilaya ya Morogoro hivyo majengo hayo yanahitaji wanafunzi ,lazima wazazi wawajibike kusomesha watoto wao.
Nsemwa anasema hata utoro kwa wanafunzi unaweza kupungua endapo watakua wanapata chakula shuleni kwani wanafunzi wengine wana umri mdogo wanahitaji kula chakula ili mwili uweze kufanya kazi.