Umoja wa Mataifa Jumanne umeonya kuwa baa la njaa linaendelea kuenea Afrika Magharibi ambako takriban watu milioni 48 wapo kwenye hatari ya ukosefu wa chakula, ikiwa idadi kubwa zaidi ndani ya kipindi cha miaka 10.
Wameongeza kusema kwamba kwa mara ya kwanza watu 45,000 waliopo kwenye eneo la Sahel wanaelekea kukabiliwa na uhaba wa chakula wakiwa hatua moja kuelekea kwenye baa la njaa. Maafisa hao wameongeza kwamba 42,000 ya watu hao ni kutoka Burkina Faso.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, hali hiyo imechochewa pakubwa na ghasia pamoja na athari za kiuchumi kutokana na janga la Corona.
Maafisa wa UN wakati wakizungumza na wanahabari kwenye mji mkuu wa Senegal, Dakar wamesema kwamba mfumuko wa bei za bidhaa pamoja na ukosefu wa usalama wa chakula zimeathiri zaidi mataifa ya Burkina Faso, Mali, Niger, kaskazini mwa Nigeria na Mauritania.
Ghasia kutokana na makundi ya kigaidi ya al Qaida na Islamic State zimeiathiri Burkina Faso na Mali kwa miaka kadhaa sasa.