Rais Emmerson Mnangagwa katika hotuba yake siku ya Jumanne, alionya dhidi ya sauti,za kigeni au za ndani, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyo ya uaminifu ambayo yanachochea migawanyiko na mifarakano.
Rais huyo, mwenye umri wa miaka 80, ambaye atawania katika uchaguzi huo wa urais unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti lakini tarehe yake bado haijathibitishwa, katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 43 ya uhuru wa taifa hilo, alitoa wito wa ‘kutojihusisha na vurugu, kabla, wakati na baada ya uchaguzi’.
Bunge lilipitisha sheria yenye utata mapema mwezi Februari inayozuia kwa kiasi kikubwa uhuru wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na kuyaweka chini ya udhibiti wa serikali na chini ya vikwazo vinavyowezekana.
Serikali yangu imechukua hatua kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika,” alisema
Historia ya kisiasa ya nchi hii ya kusini mwa Afrika inaangaziwa na vurugu na vitisho wakati wa uchaguzi. Akiingia madarakani mwaka wa 2017 katika mapinduzi dhidi ya gwiji mkuu wa nchi hiyo, Robert Mugabe, Bw. Mnangagwa alishinda uchaguzi wa urais mwaka uliofuata kwa asilimia 50.8 ya kura.
Chama cha mpinzani wake mkuu, Nelson Chamisa, 45, kinamtuhumu kwa kuwakandamiza wapinzani wa kisiasa. Katika wiki za hivi karibuni, mikutano ya upinzani imezuiwa na viongozi wakiwemo wabunge kukamatwa.
Emmerson Mnangagwa ambaye ameshindwa licha ya ahadi za kurejesha uchumi unaodorora kwa miaka ishirini, anakabiliwa na hasira za wananchi.