Makumi ya watu waliuawa katika msongamano uliopelekea mkanyagano wa watu katika mji mkuu wa Sanaa nchini Yemen mapema wiki hii wakati wakazi wenye mahitaji katika taifa hilo lililokumbwa na vita wakimiminika kupokea misaada kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo hilo wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Takriban watu 78 waliuawa katika tukio hilo kusikitisha na wengine kadhaa kujeruhiwa, Mutahar al-Marouni, mkurugenzi wa ofisi ya Afya inayoendeshwa na Wahouthi jijini Sanaa, aliliambia shirika la habari la Al-Masirah. Kulingana na taarifa ya shirika la habari la Reuters, mamia ya watu walikuwa wamejazana katika shule ili kupokea misaada ambayo iliripotiwa kuwa takriban $9 (Tzs 21,114) kwa kila mtu.
Tukio hilo lilitokea siku chache tu kabla ya sikukuu ya Eid al-Fitr, ambayo inaadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mamlaka Kuu ya Zakat inayoongozwa na chama cha Houthi ilitangaza katika taarifa yake kuwa itatoa Riyal milioni moja ya Yemeni ($4,000) ambayo ni takriban Tzs 9,384,000 kwa kila familia ya wahanga wa tukio hilo na pia ilisema itagharamia matibabu ya wote waliojeruhiwa na kulipa Riyal 200,000 ya Yemen ($800) (Tzs 1,876,800) kwa kila mtu aliyejeruhiwa.