Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo amekabidhi baiskeli 200 kwa Wanafunzi wa kike kwa Shule 10 za Sekondari Wilayani humo ambapo amesema zitawasaidia Vijana wa kike kufika Shuleni kwa wakati na kuondokana na utoro kwa kutokufika Shule mara kwa mara kutokana na umbali mrefu wanaotembea kutoka majumbani mwao hadi kufika Shuleni.
Akiongea wakati wa hafla maalum ya makabidhiano ya baiskeli hizo ambazo zimetolewa na Shirika la Uratibu na Ushirikano la Uturuki (TIKA) chini ya Ubalozi wa Uturuki Nchini Tanzania, DC Jokate amesema….“Sisi tunawashukuru sana Mh. Balozi wa Ututuki kwa kuunga mkono juhudi za Mh. Rais Dkt. Samia katika kuboresha mazingira ya elimu kwa Mtoto wa kike, kwakweli mmepanda mbegu ambayo inaishi kwa Watoto wetu na hii mmetoa hamasa kwao kuweza kusoma kwa bidii zaidi”
“Na ndio maana nimesisitiza hawa Watoto huko Shuleni wakazane na masomo watumie baiskeli hizi kwenda Shule na kurudi nyumbani kuwasaidia Wazazi wao na sio kuzitumia kwenye matumizi yasiyo sahihi”
Kwa upande wake Balozi wa Uturuki hapa Nchini Dr. Mehment Gulluoglu amesema lengo la kukabidhi baiskeli hizo ni kuwasaidia Watoto kutokutembea umbali mrefu kufuata elimu na hivyo baiskeli hizo zitawasaidia kufika Shule kwa wakati na kufanya vizuri kwenye masomo yao.