Polisi wa Haiti Jumatatu wamesema kwamba takriban watu 10 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la wahalifu waliuawa kwa kupigwa vibaya na miili yao kuchomwa moto na wakazi wa mji wa Port-au-Prince.
Msemaji wa polisi Gary Desrosiers amesema kundi la majambazi wenye silaha lililikuwa likisafiri kwa gari katika mji mkuu na kwamba polisi walikuwa na nia ya kuwakamata.
Mauaji hayo yanafuatia siku kadhaa za makabiliano kati ya wanachama wa magenge na maafisa wa usalama.
Picha za Reuters na video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha miili kadhaa ikiwa imerundikana barabarani, huku matairi yenye moshi na vifaa vingine vikiwa juu ya miili hiyo.
Magenge ya wahalifu nchini Haiti yamekuwa na nguvu zaidi tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moise mwaka wa 2021, huku wakazi wakijipata katika mapambano kati ya magenge hayo wakati sehemu kubwa ya mji mkuu na mikoani ikikabiliwa na ukosefu wa utawala wa sheria.
Katika muda wa siku sita tu, kati ya tarehe 14 na 19 Aprili, karibu watu 70 waliuawa katika mapigano yaliyohusisha magenge katika mtaa mkubwa wa mabanda wa Port-au-Prince, Cité Soleil, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu. Takriban 40 kati ya waliofariki walipigwa risasi au kudungwa visu. Angalau wawili walikuwa watoto.