Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimeendesha Semina ya Kuwajengea Uwezo Wafanyakazi Vijana ikiwa ni shughuli za Chama hicho kuelekea Maadhimisho ya Mei Mosi 2023 yatakayofanyika Kitaifa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Semina hiyo ilihusisha Vijana takribani 100 kutoka sehemu mbalimbali za kazi mkoani Morogoro ili kuwajengea uwezo kuhusu Shughuli za Vyama vya Wafanyakazi, Viwango vya Ajira na Umuhimu wa Mikataba ya Pamoja katika Kuimarisha Uhusiano Bora Maeneo ya Kazi na Ajira za Staha.
Akifungua Semina hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUICO Ndugu Paul Sangeze amesema Chama cha Wafanyakazi TUICO kinatambua umuhimu wa Kundi la Vijana ndani ya Chama na ndio maana kimeendelea kulipa nafasi kundi hilo.
“Chama kinawategemea vijana katika kukijenga na kukilinda. Ninawasihi mshiriki katika kampeni za uhamasishaji ili vijana wengine wajiunge. Mjitokeze kunapokuwa na nafasi za uchaguzi katika ngazi mbalimbali ili kujenga uzoefu mkubwa wa uongozi katika vyama vya wafanyakazi,” alisema Paul Sangeze, Mwenyekiti TUICO Taifa.
“Kipaumbele chetu ni elimu kwa vijana. Ni katika kundi hili tutapata viongozi wa baadaye wa vyama vya wafanyakazi. Hivyo tumewaita hapa, tukiwa tuaelekea Mei Mosi 2023 ili tubadilishane uzoefu kuhusu vijana na vyama vya wafanyakazi. Tunaamini mkitoka hapa mtakuwa chachu katika shughuli za TUICO kwenye maeneo yenu ya kazi,” alisisitiza Boniface Nkakatisi, Katibu Mkuu TUICO.
TUICO kinatekeleza shughuli mbalimbali kuelekea Mei Mosi 2023 ambapo kimeanza na Semina ya Wafanyakazi Vijana na baadaye wiki hii kitakutana na Viongozi Waandamizi wa Taasisi za Kazi na Wafanyakazi Wanawake na kushiriki Maonesho ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi kuanzia Aprili 26, 2023 katika Viwanja vya Tumbaku, Mkoani Morogoro.