Ujumbe wa Wataalam kutoka Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii kutoka Kenya umehitimisha ziara yake ya siku nne nchini iliyolenga kubadilishana uzoefu kuhusu sheria na taratibu mbali mbali za kazi ambapo wamesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa masuala ya kazi hususan mifumo ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi.
Akiongea mara baada ya kuhitimisha ziara yao katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi ya Kenya, Bw. Geoffrey Kaituko, amesema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitafuta uzoefu wa mambo mbali mbali ughaibuni ilihali uzoefu huo unapatikana katika nchi zinazowazunguka.
“Ziara yetu hapa Tanzania imekuwa ya kufana sana, tumetembelea Taasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kwahiyo sisi tumefurahi sana kwa mapokezi mazuri tuliyoyapata pamoja na mambo mazuri tuliyojifunza.
Mara nyingi tumekuwa na mazoea ya kwenda Ulaya kujifunza mambo fulani fulani mfano kwa mambo haya ya OSHA tungetaka kwenda Ujerumani wakati hapa Tanzania kuna Taasisi nzuri sana inayosimamia masuala ya usalama na afya hivyo jambo ambalo tunatoka nalo hapa ni kwamba nasisi ni lazima twende tukaanzishe Taasisi kama hii,” amesema Geoffrey Kaituko.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu, amesema kupitia ziara hiyo ya wataalam kutoka Kenya, Ofisi yake imejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi walivyofanikiwa kuwezesha watu wao kupata ajira nje ya nchi yao na hivyo kuliingizia Taifa lao fedha nyingi za kigeni.
“Mfano katika suala la Wakenya wanaofanya kazi nje yan chi yao, Saudi Arabia wana wafanyakazi zaidi ya 120,0000, Qatar zaidi ya wafanyakazi 60,000 na nchi nyingine za Kiarabu zaidi ya 40,000 hivyo nimejifunza kwamba fedha wanayopata kutoka nje kutokana na ajira za nje ni zaidi hata ya fedha zinazotokana na mazao yao makuu ya biashara kama vile Kahawa na Chai.