Mchungaji maarufu nchini Ezekiel Odero amewasilishwa katika mahakama ya Shanzu pwani ya Kenya huku maofisa wa polisi wakitaka azuiliwe kwa siku 30 zaidi wakati huu uchunguzi ukiendelea.
Kwa mujibu wa maofisa wa upelelezi, watu waliofariki wakiwa katika kanisa la mhubiri huyo walizikiwa katika shamba Shakahola ambako kumefukuliwa zaidi ya miili 90, shamba linalohusishwa na mchungajimwenye imani tata Paul Makenzie anayeshikiliwa na polisi pia.
Ezekiel Odero ambaye ni kiongozi wa kanisa la New Life Prayer Centre and Church, alikamatwa siku ya Alhamisi, akitarajiwa kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu kwa mujibu wa taarifa ya waziri Kindiki.
Odero amefikishwa mahakamani wakati huu uchunguzi ukiendelea dhidi ya Paul Mackenzie Nthenge, mhubiri ambaye anadaiwa kuhusika na vifo vya watu 98 ambao ni washirika wa mafunzo yake.
Wafuasi wa Makenzie wanadaiwa kufariki baada ya kufunga kula chakula kwa maagizo ya kiongozi huyo wa dini wakiwa na nia ya kukutana na Yesu Kristo kwa haraka.
Wakati akisafirishwa kutoka makao makuu hayo ya kanisa kwenda makao makuu ya polisi yaliyoko Mombasa kwa ajili ya mahojiano. Odero, alikuwa amevalia vazi lake maalumu jeupe na akiwa ameshika Biblia.
“Watu hukusanyika kanisani kwangu kwa sababu mimi ndiye niliyechaguliwa,” aliakiambia kituo cha habari cha NTV mwezi Desemba mwaka jana
Odero anadai kuwa nguo chakavu kuwa ni “takatifu” pamoja na maji yanauzwa kwenye mikutano yake mikubwa kwa shilingi 100 za Kenya yanauwezo wa kuponya ugonjwa wowote, ikiwa ni pamoja na UKIMWI.
Anajivunia chaneli yake ya YouTube yenye watumiaji takriban watu 450,000 ikiwa imejaa ushuhuda wa Wakenya wanaodai kuponywa na Odero – kuanzia wagonjwa wa saratani walioponywa kupitia maombi hadi vipofu wanaoweza kuona tena.