Maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Dei yaliyofanyika jana nchini Italia yalikuwa tofauti na ya nchi zingine barani Ulaya baada ya waandamanaji wenye hasira kuchoma bendera za Umoja wa Ulaya EU na za Shirika la Kjeshi la NATO zilizoko nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRNA washiriki wa maandamano ya Siku ya Wafanyikazi Duniani yaliyofanyika mjini Rome walichoma bendera za Umoja wa Ulaya na NATO kuonyesha upinzani wao dhidi ya hatua ya kutuma silaha na zana za vita huko Ukraine na msaada wa kifedha kwa serikali ya Kiev.
Mjini Turin, Italia, waandamanaji wanaoipinga serikali waliandamana wakiwa wameshikilia wanasesere kumdhihaki Waziri Mkuu wa nchi hiyo Giorgia Meloni huku katika mji wa Potenza kusini mwa Italia, wafanyakazi walimiminika barabarani kupinga serikali ya mrengo wa kulia ya Waziri Mkuu Meloni.
Mwaka uliopita pia wakati wa maandamano ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, maelfu ya waandamanaji nchini Italia waliitaja NATO kuwa ni shirika la kigaidi na kutoa nara na kaulimbiu dhidi ya sera za shirika hilo la kijeshi na uungaji mkono wake kwa vita vya Ukraine na vikwazo lilivyoiwekea Russia.
Hapo jana, na sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Dei, katika nchi nyingine za Ulaya kama Ufaransa, Ujerumani, Uswisi, Uingereza na Uholanzi, yalifanyika maandamano makubwa ya wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi vya nchi hizo.
Polisi wa Ufaransa walikabiliana na waasi waliovalia mavazi meusi wakati wa mikutano ya Mei Mosi.
Kote Ufaransa baadhi ya watu 800,000 waliandamana amesema waziri wa mambo ya ndani Gerald Darmanin.
Waliandamana kupinga hatua ya karibuni ya rais Emmanuel Macron ya kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 mpaka 64.
Waandamanaji wanaona hilo ni tishio kwa haki za wafanyakazi huku Macron akisema ni mahitaji ya kiuchumi kutokana na watu wengi kuwa na umri mkubwa.