Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya chakula limesitisha kusambaza misaada katika mkoa wa kaskazini wa Ethiopia, Tigray.
Hatua hiyo imefanyika ikiwa ni katikati ya uchunguzi kuhusu wizi wa chakula ambacho kilipaswa kupewa watu wenye njaa kwa mujibu wa wafanyakazi wanne wa misaada.
Mpango huo wa chakula duniani (WFP) unahusika na kusambaza chakula kutoka Umoja wa Mataifa na washirika wengine kwenda Tigray katikati mwa vita vya miaka miwili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo malizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Novemba.
Zaidi ya watu milioni 5 wa eneo hilo lenye watu milioni 6 wanategemea misaada.
Mwezi uliopita shirika la habari la AP liliripoti kwamba WFP ilikuwa inachunguza madai ya matumizi mabaya ya chakula na kupelekwa kusiko stahiki nchini Ethiopia, ambapo watu milioni 20 wanahitahi misaada ya kibinadamu kutokana na ukame na mgogoro.
WFP iliwasiliana na washirika wake wa kimisaada Aprili 20 na kuwaeleza kwamba inasimamisha usambazaji wa chakula mkoani Tigray, mmoja wa wafanyakazi wa utoaji misaada aliliambia shirika la habari la AP.
Barua iliyotumwa na mkurugenzi wa Ethiopia wa WFP mnamo Aprili 5 iliwataka washirika wa kibinadamu kushiriki “taarifa yoyote au kesi za matumizi mabaya ya chakula, ubadhirifu au upotoshaji ambao unafahamu au unaoletwa kwako na wafanyakazi wako, walengwa au mamlaka za mitaa.”
Wakati huo, wafanyakazi wawili wa misaada waliiambia AP kwamba vifaa vilivyoibiwa vinajumuisha chakula cha kutosha kulisha watu 100,000. Chakula hicho kiligunduliwa hakipo kwenye ghala katika mji wa Tigray wa Sheraro. Haikujulikana ni nani aliyehusika na wizi huo.
Rais mpya wa mpito wa Tigray, Getachew Reda, alisema mwezi uliopita alijadili “changamoto inayoongezeka ya upotoshaji na uuzaji wa chakula cha msaada kwa ajili ya wahitaji” na maafisa wakuu wa WFP wakati wa ziara ya shirika hilo huko Mekele, mji mkuu wa kanda.
Msemaji wa WFP nchini Ethiopia hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni yake