Umoja wa Mataifa, umeonya kuwa huenda watu zaidi ya laki 8 wakakimbia mapigano na hali mbaya ya kibinadamu nchini Sudan, wakati huu licha ya makubaliano ya usitishaji mapigano, kumeripotiwa makabiliano mjini Khartoum na kwenye miji mingine.
Mapigano yameendelea licha ya pande zote mbili zinazopambana kukubaliana kuacha mapigano, kwa saa 72. Umoja wa Mataifa unasema, hali ya kibinadamu inaendelea kuwa mbaya.
Kwa wiki ya tatu sasa, mapigano yameendelea, huku zaidi ya watu Elfu 50 wakikimbia makaazi yao na kuvuka mpaka kwenda katika nchi jirani za Misri, Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Wakaazi wa Khartoum wanasema, wanashuhudia ndege za kivita na kusikia milio ya risasi, huku wakilalamikia ukosefu wa mahitaji muhimu kama chakula, maji na dawa.
Raia wa kigeni wameendelea kuondoka nchini humo kuanzia wiki iliyopita, huku watalaam wakiripoti kuwa watu zaidi ya 500 wameuawa tangu kuanza kwa mapigano hayo Aprili 15.
Onyo hili la UN linakuja wakati huu nchi jirani na Sudan zinazoendelea kupokea wakimbizi kama vile Chad zikiwa katika hatari ya kukabiliwa na mzozo wa kiuchumi kutokana na idadi kubwa ya raia wanaoingia katika mataifa hayo.
Wito umezidi kutolewa kwa pande zinazohasimiana nchini Sudan kusitisha mapigano kama njia moja ya kuliepusha taifa hilo kutumbukia katika machafuko.