Kanali Charles Okello Engola, Waziri wa nchi katika masuala ya Ajira, Leba na Mahusiano ya Viwanda ameuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi wake mapema leo Jumanne asubuhi wakati alipokuwa anaingia kwenye gari lake kuelekea kazini.
Jeshi la Polisi la Uganda limethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, waziri huyo amepigwa risasi nyumbani kwake Kyanja na mlinzi wake mmoja ambaye inadaiwa alifyatua risasi kadhaa akiwa karibu naye.
Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, Fred Enanga amewaambia waandishi wa habari jijini Kampala kwamba mlinzi huyo ametambuliwa kwa jina la Pte Wilson Sabiiti.
Amesema, baada ya kufanya mauaji hayo, mlinzi huyo ametoroka kutoka eneo la mauaji na kukimbia hadi kwenye kituo cha biashara cha Kyanja, kilichoko Ring Road ambako aliingia kwenye saluni na kuamua kujipiga risasi na kujiua.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Uganda, Meja Jenerali Geoffrey Tumusiime Katsigazi na mkurugenzi wa kitengo cha upelelezi (CID), Meja Tom Magambo ndio maafisa wa kwanza wa ngazi za juu waliofika nyumbani kwa waziri huyo na zoezi la kutafuta vielelezo zaidi ambavyo vitasaidia uchunguzi wa polisi, limeanza papo hapo.
Bw. Fred Enanga pia ametofa ufafanuzi zaidi akisema: “Uchunguzi kwa sasa uko katika hatua za awali. Pia tumetuma timu ya wataalamu kwenye eneo la uhalifu ambao wanatumia teknolojia ya hali ya juu zaidi ya upelelezi ili kupata ni nini hasa kimesababisha mauaji haya mabaya. Hatutaki kukisia sababu hasa ya kupigwa risasi waziri hayo hadi tuthibitishe na tujiridhishe.”
PLAY:WAZIRI APIGWA RISASI NA MLINZI WAKE, “SIJALIPWA MSHAHARA MUDA MREFU”