Michezo ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi na yenye mvuto mkubwa na wapenzi wengi nchini Tanzania, kutokana na umuhimu na mchango wake unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Sekta hii inayoongozwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuwa kiungo muhimu cha kuwaburudisha na kuwapa furaha Watanzania wapatao 61,741,120 (milioni 61.74), kuwawezesha kuwa na uchangamfu na afya njema, lakini pia kukuza ajira nchini Tanzania.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza shughuli za Michezo nchini ikiwa ni pamoja na kuziwezesha na kuzigharamia Timu mbalimbali za Taifa kushiriki mashindano ya kimataifa.
Mathalan, Timu ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) ilishiriki Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17 nchini India Oktoba, 2022. Kupitia maandalizi yaliyogharamiwa na Serikali, timu hiyo iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kushiriki ngazi ya Kombe la Dunia kwenye Soka la Wanawake.
Pia Vilabu vikubwa na maarufu nchini Tanzania na Ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati vya Simba na Yanga vinashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Nayo Timu ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) kwa mara ya kwanza ilishiriki na kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali za Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu duniani nchini Uturuki Septemba, 2022 na kuiweka Tanzania katika nafasi ya saba kati ya timu kumi Bora za dunia.
Isitoshe, baada ya miaka mingi, Tanzania ilifanikiwa kupata medali tatu; mbili za shaba na moja ya fedha katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola, yaliyofanyika mwaka 2022, Birmingham, Uingereza ambapo Mwanariadha Francis Simbu alipata medali ya fedha na medali mbili za shaba kutoka kwa Mabondia Yusuph Changarawe na Kassim Mbundikwe.
Aidha, katika kuimarisha na kuwa na timu bora za Taifa, msingi mkuu ni kuibua na kuendeleza vipaji. Katika hili Serikali inaendeleza mashindano ya kuibua vipaji vya wanamichezo wanafunzi maarufu kama UMISSETA na UMITASHUMTA. Pia inaendelea kuboresha miundombinu ya michezo kwa kutoa msamaha wa Kodi kwenye nyasi bandia za viwanja vya michezo ili kutoa fursa ya Watanzania kuendelea kunufaika na uwepo wa viwanja bora vya michezo.