Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini jana ilitoa taarifa na kutangaza kuwa pande zinazozozana hko Sudan zimekubaliana kutekeleza usitishaji vita mpya nchini humo.
Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo chini ya uongozi wa Jenerali Abdul Fattah al-Barhan ambaye ni mkuu wa baraza la uongozi la Sudan na Mohammed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la “Hamidati” kamanda wa vikosi vya radiamali ya haraka (RSF).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini ilisema jana kupitia taarifa yake kwamba: Imefanya mazungumzo ya simu na al Burhan na Hamidat na kwamba pande hasimu zimekubaliana katika hatua ya awali kurefusha usitishaji vita huko Sudan.
Taarifa ya wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini imebainisha kuwa, usitishaji vita huo wa mapigano utatekelezwa kwa wiki moja kuanzia Alhamisi tarehe 4 hadi 11 mwezi huu wa Mei. Wakati huo huo, Volker Peretz, Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, amesema:Mazungumzo yatakayofanyika kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya radiamali ya haraka si ya kisiasa, bali ni ya kiufundi, na kwamba, mlango wa mazungumzo umefunguliwa kwa ajili ya kusitisha mapigano huko Sudan.
Mapigano huko Sudan yameingia katika wiki ya tatu ambapo jana Jumanne vikosi vya radiamali ya haraka vilitangaza kuitunguka ndege ya kivita ya jeshi la nchi hiyo aina ya MIG.