Takriban watu wanane wamekufa kusini magharibi mwa Uganda katika wilaya ya Kisoro baada ya nyumba zao kufunikwa na maporomoko ya matope.
Maporomoko hayo yalisababishwa na mvua za vipindi, shirika la Msalaba Mwekundu limesema Jumatano wakati wafanyakazi wa misaada na wakaazi wa eneo wakifukua matope kutafuta miili ya watu.
Watu sita kati ya wanane wanatoka familia moja ambayo nyumba yao ilifunikwa na maporomoko hayo.
Afisa mwandamizi wa wilaya ya Kisoro, Abel Bizimana amesema mabadiliko ya hali ya hewa, kilimo duni na usimamizi mbaya wa udongo vinastahili kulaumiwa kwa maporomoko hayo ya matope.
Kwa mujibu wa shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda wengi wa waliokufa ni wanawake na watoto.
Uganda kama ilivyo katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki imekuwa na mvua kubwa. Meneja wa mawasilinao wa shirika la Msalaba Mwekundu Uganda amesema juhudi za kuwasaidia walioathirika zinaendelea.
Wakati huohuo Rwanda inaomboleza leo vifo vya watu 130 waliofariki kutokana na mafuriko makubwa na maporomoko ya matope yaliyoharibu pia nyumba za watu na kusababisha wengi wao kukosa makazi.
Serikali bado inahesabu gharama za uharibifu wakati familia zikijiandaa kuwazika jamaa zao baada ya janga hilo la kiasili lililosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya mwinuko na milimani.