Gavana wa Kivu Kusini katika Jamhurii ya Kidemokrasia ya Congo, Théo Ngwabidje Kasi, amesema idadi ya waliofariki dunia imefikia 176 na kwamba wengine wengi bado hawajulikkani walipo.
Hata hivyo mwanachama wa jumuiya ya kiraia katika eneo hilo, Kasole Martin, amesema miili 227 ya walioaga dunia kutokana na mafuriko imepatikana.
Vijiji vya Bushushu na Nyamukubi – vilisombwa na maji baada ya mito ya mashariki mwa Congo kuvunja kingo zake.
Kasole Martin amesema: “Watu wanalala nje, na shule na hospitali zimefagiliwa.”
Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba katika mojawapo ya vijiji vya Kivu Kusinii zaidi ya robo tatu ya nyumba zote zimesombwa na maji ikiwa ni pamoja na vituo vya afya na shule.
Upande wa pili wa Ziwa Kivu katika nchi jirani ya Rwanda watu 130 wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo.
Ripoti zinasema, wanafunzi 15 ni miongoni mwa waliofariki dunia, na kwamba jumla ya shule 33 zimeharibiwa. Nyumba zisizopungua 500 pia zimeharibiwa na mafuriko ya wiki hii nchini Rwanda hususan katika Wilaya za Rubavu, Karongi, Rutsiro, Nyabihu na Ngororero ambazo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo.