Leo kumefanyaika uzinduzi wa Kitabu kinachojulikana kwa jina la Sonona Kazini ambapo mwanadada Grace Mapenda amekitambulisha kitabu hicho kikiwa na lengo la kutatua changamoto kwa watu wenye matatizo ya Sonona.
Mbali na hilo Grace Ameeelza namna Kitabu hicho kitakavyo kwenda kuleta tija kwa jamii huku akitoa maelekezo ya namna ya kukipata Kitabu hicho.
‘Ninamshukuru sana Mungu kwa kibali katika siku hii kubwa ya leo, ninaishukuru sana familia yangu katika kuhakikisha ndoto yangu ya uzinduzi wa kitabu inatimia lakini pia ninajishukuru mimi mwenyewe kwa kuhakikisha natimiza kile nilichobeba kwa utukufu wa Mungu na kwa upekee kabisa ninakushukuru wewe kwa kuweza kufika mahali hapa katika uzinduzi huu’- Grace Mapenda
‘Sonona ni moja kati ya vipaumbele vya shirika la afya duniani kupitia mpango mkakati uitwaio WHO’s mental health Gap Action Programme (mhGAP) ikilenga kusaidia nchi mbalimbali haswa kwa nchi za kipato cha chini na kati kuongeza utoaji huduma juu ya afya ya akili na magonjwa mbalimbali ya mfumo wa fahamu’- Grace Mapenda
‘Sonona inafanya kazi ndani yetu tukiwa kazini, nyumbani. kwenye biashara, kwenye familia, kwenye mahusiano yetu, mashuleni. Sonona inafanya kazi katika kila sehemu ya maisha yetu’- Grace Mapenda
‘Ni muhimu kutambua kwamba sonona sio udhaifu wa kibinafsi au chaguo. Ni hali ya kiafya inayohitaji utambuzi na matibabu sahihi. Sonona inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maumbile, matukio ya maisha, na kutofautiana kwa kemikali katika ubongo na mengineyo mengi. Ni muhimu kwa waajiri kuelewa athari za sonona kwa wafanyikazi wao na kuchukua hatua za kuwaunga mkono mapema iwezekanavyo’- Grace Mapenda
‘Ni muhimu kukumbuka kuwa sonona inaweza kumpata mtu yeyote wa hali yeyote, mahali popote na ni hali inayoweza kutibika na kupona. Kama viongozi na washawishi katika nyanja zetu husika, ni muhimu kukuza utamaduni wa ufahamu na msaada wa afya ya akili’- Grace Mapenda
Hii ni pamoja na kuunda mazingira ya kazi ambayo yanatanguliza afya ya akili, mazingira ambayo ni rafiki kwa kufanya kazi na kujifunza, vilevile mazingira ambayo viongozi husika wa maeneo hayo watafanya kazi kwa weledi bila kubagua au kushusha thamani ya mtu kutokana na wadhifa wake au kipato chake, mazingira yenye usawa wa kijinsia na kiimani, pia kutoa nyenzo kama vile huduma za ushauri nasaha au programu za usaidizi kwa wafanyakazi na kuhimiza mawasiliano ya wazi kuhusu changamoto za afya ya akili na kutekeleza mipango ya kazi inayoweza kunyumbulika au likizo ili kushughulikia matibabu.
Kitabu hiki kina lengo la kuleta suluhisho la tatizo hili hasa ikilenga jamii ya vijana ambao ni waathirika wakubwa wa ugonjwa huu na hii ni kutokana na ukweli kwamba changamoto za kimaisha na mabadiliko ya kitehama ikiwa ni pamoja na kuiga tamaduni za magharibi pamoja na mambo mengi yasiyokua na uhalisia. Kitabu hiki pia kimelenga kusaidia kutoa elimu kuhusu Afya ya akili hususani Sonona ambayo ni moja kati ya magonjwa yanayokuwa kwa kasi kubwa zaidi.
Pia kutengeneza njia ya kupata matibabu na namna ya kujikwamua kwa wale wote walioathirika na sonona.
‘Tunatarajia kutoa nakala takribani 1,000 bure kwa vijana katika elimu ya juu (vyuo vikuu), ikiwa ni vitabu 50 kwenye kila maktaba ya chuo na vitabu 30 kwenye kila nyumba ya upataji nafuu (sober house) pamoja na matarajio ya kufikia vyuo 14 na 10 sober house, hivyo kutokana na gharama za usambazaji tunatarajia kuanza na mkoa wa Dar Es Salaam mapema baada ya uzinduzi wa kitabu hiki’- Grace Mapenda
“Tunatambua na tunathamini jitihada zote mnazozifanya kama Serikali ya awamu ya sita katika kupambana na changamoto za afya ya akili na tunatoa pongezi zetu za dhati. Tunaamini kwa msaada wako mkubwa ukiwa kama kiongozi wa juu wa mkoa wa DSM tutaweza kufikia malengo ya kuwasaidia watanzania wenzetu kulinda afya ya akili hasa vijana ambao ni taifa la leo na kesho”- Grace Mapenda
“Kwa pamoja tushirikiane kuunda mazingira ya kazi ambayo ni bora zaidi kwa afya ya akili zetu, kuwepo kwa wafanyakazi bora kutachangia uzalishaji bora hivyo kuongeza pato la mtu binafsi, familia, taasisi na taifa kwa ujumla”- Grace Mapenda
“Ninahimiza sote kutanguliza afya zetu za akili na kuchukua hatua za kusaidia wale walio karibu nasi ambao wanaweza kuwa wanapambana na sonona au wapo katika dalili za awali za sonona”- Grace Mapenda