Uchunguzi wa kidaktari uliofanyiwa miili 112 ya wahanga wa mauaji tata ya Shakahola iliyofukuliwa katika makaburi mbalimbali katika kaunti ya Kilifi katika eneo la Pwani Kenya imeondoa uwezekano juu ya uwepo wa uvunaji viungo katika miili ya wahanga hao.
Wataalamu hao wa serikali ya Kenya waliofanyia uchunguzi miili hiyo wameeleza kuwa baadhi ya wahanga waliaga dunia kwa njaa, kukabwa koo na kukosa hewa. Mhubiri tata wa Kikristo Paul Mackenzie anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kufunga ili wawe wa kwanza kwenda mbinguni.
Polisi ya Kenya inatazamia kufukua makaburi mengine ili kuwasaka wahanga waliosalia. Mhubiri tata Mackenzie sasa anashikiliwa katika seli ya polisi huku uchunguzi ukiendelea. Wakati huo huo Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limetangaza kuwa hadi sasa watu 360 hawajulikani walipo huku wengine wasiopungua 60 wakiwa wameokolewa wakiwa hai katika sakala hilo la Shakahola.
Tayari Rais William Ruto wa Kenya ameunda tume itakayochunguza mauaji hayo tata katika msitu wa Shakahola ambao uko katika shamba linalomilikiwa na kasisi aliyehusishwa na mauaji hayo. Wakili Kioko Kilukumi ataongoza wakili mkuu na kusaidiwa na Vivian Nyambeki na Bahati Mwamuye.
Tume hiyo itachunguza vifo vya zaidi ya watu 100 wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa pote moja la Kikristo lenye misimamo mikali ambalo kiongozi wake aliwaamuru wakae na njaa hadi kufa ili waweze kukutana na Yesu mbinguni, msemaji wa rais Ruto alisema.
Kulingana na notisi iliyotolewa kwenye gazeti la serikali, tume hiyo itatayarisha ripoti chini ya miezi sita na kutoa mapendekezo yao kwa Rais Ruto. Tume hiyo ina jukumu la kubainisha chanzo cha vifo vilivyotokea na pia kuchunguza ni nini kilichosababisha idara za usalama, usimamizi na sheria kufeli kuchukua hatua hadi maafa kutokea.