Vyama vitatu vya upinzani vya Kongo Brazzaville vimeitisha mkutano wao wa kwanza ndani ya muungano wao ili kuelezea malengo ya kundi hilo kabla ya uchaguzi wa 2026. Shabaha kubwa ya muungano huo ni kumuondoa madarakani Rais Denis Nguesso, ambaye amekuwa akiitawala nchi hiyoi tangu mwaka 1997.
Muungano huo mpya unaojulikana kwa jina la Alliance for Democratic Alternation mwaka wa 2026 (2AD2026), unaundwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo cha Rais wa zamani Jacques Joachim Yhomby Opango, na vyama vingine viwili vya Movement of Republicans na People’s Party.
Vyama hivyo vina uungwaji mkono wa mashinani lakini havina viti bungeni.
Mkuu wa kwanza wa muungano huo ambaye ni kutoka chama cha Movement of Republicans, Destin Gavet, amesema kuwa, kazi waliyoifanya hivi sasa imewawezesha kupasisha maafikiano maalumu, na zaidi ya yote imewawezesha kujiwekea malengo ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu.
Amesema mapendekezo kadhaa pia yametolewa ili kushughulikia suala la wafungwa wa kisiasa, wakiwemo Jean-Marie Michel Mokoko na André Okombi Salissa. Ameongeza kuwa, kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa kunaweza kuwa njia ya kupunguza wasiwasi wa kisiasa na zaidi ya yote kukuza mshikamano wa kijamii na umoja wa kitaifa.
Wakuu hao wawili wa upinzani wamefungwa kwa madai ya kudhoofisha usalama wa ndani ya Kongo Brazzaville baada ya uchaguzi wa 2016. Uchaguzi huo ulifuatiwa na vurugu na kusababisha vifo vya watu 17 baada ya wapinzani kumtuhumu Rais Nguesso kuwa alichakachua matokeo ya uchaguzi na kujitangaza mshindi kwa asilimia 67 ya kura. Muungano wa upinzani ulizinduliwa mwezi Aprili mwaka huu kwa lengo la kuleta mabadiliko katika hali ya kisiasa inayodhibitiwa na Nguesso hivi sasa.