Zadi ya watu mia tano wamefariki dunia kutokana na mafuriko na kufunikwa na maporomoko ya matope yaliyosababishwa na na mvua kubwa za siku nne mfululizo huko Nyamukubi wilayani Kalehe katika jimbo la Kivu kusini.
Mvua hizo pia zimesababisha uharibifu wa nyumba, ni moja ya maafa makubwa sana katika historia ya hivi karibuni huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Manusura walitazama video zilizochapishwa mitandaoni zikiwaonyesha wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wakirundika maiti kwenye makaburi mapya ya halaiki yaliyochimbwa mwishoni mwa wiki.
Wafanyakazi hao wametumia siku kadhaa kuopoa miili iliyojaa matope kutoka katika vijiji vya Bushushu na Nyamukubi vilivyopo katika mkoa wa Kivu Kusini, ambako mvua kubwa ya siku kadhaa ilisababisha maporomoko ya udongo na mito kuvunja kingo siku ya Alhamisi.
“Tuliacha kila kitu nyuma,” alisema mkazi wa Bushushu, Bahati Kabanga mwenye umri wa miaka 32, ambaye alifanikiwa kumuokoa mtoto wake pekee lakini aliwapoteza shangazi, dada na wapwa zake.
“Tulihisi tetemeko wakati mvua alipokuwa ikinyesha, tukaamua kukimbia baada ya kuona nyumba kwa mbali zikiporomoka,” aliliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.
Serikali kuu mjini Kinshasa bado haijatoa idadi ya vifo. Imetuma wajumbe kwenye eneo hilo na kutangaza Jumatatu siku ya maombolezo ya kitaifa.
Hali ya joto kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa inazidisha kiwango cha mvua za mara kwa mara barani Afrika, kulingana na wataalam wa hali ya hewa wa Umoja Wa Mataifa.
DRC inaendelea kukabiliwa na athari mbaya za mafuriko kote nchini. Mwezi Desemba, zaidi ya watu 120 waliuawa baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko katika mji mkuu wa Kongo wa Kinshasa, mamlaka ilisema.
Mwaka 2020, zaidi ya nyumba 15,000 ziliharibiwa na takriban watu 25 waliuawa na mafuriko huko Kivu Kusini, jimbo ambalo tayari limeharibiwa na vita, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa liliripoti wakati huo.
Miezi kadhaa mapema, karibu watu 39 walikufa wakati mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi huko Kinshasa.