Jumuiya mbalimbali za kisiasa nchini Mali zimeunganisha nguvu pamoja ili kupinga uamuzi wa serikali ya kijeshi ya nchi hiyo wa kuendesha kura ya maoni kuhusu katiba mpya nchi hiyo ambapo kura hiyo ya maoni imepangwa kufanyika Juni 18 mwaka huu.
Kura hiyo ya maoni iliyotangazwa Ijumaa iliyopita ni hatua muhimu katika njia ya nchi kuelekea uchaguzi ulioahidiwa na wanajeshi baada ya mapinduzi ya miaka mitatu iliyopita. Awali serikali ya kijeshi ya Mali ilipanga kura hiyo ya maoni ifanyike Machi 19 mwaka huu, hata hivyo iliakhirishwa.
Muungano huo wa kisiasa nchini Mali unataka kufutwa uamuzi huo wa kuitisha kura ya maoni na katiba ukiamini kuwa mamlaka iliyoko madarakani inatawala kinyume cha sheria. Muungano huo aidha umeeleza kuwa zaidi ya theluthi mbili ya ardhi ya Mali inasumbuliwa na hali ya ukosefu wa usalama kwa ujumla.
Kwa muda mrefu sasa mijadala mbalimbali imekuwa ikifanyika huko Mali kuhusu suala la kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.
Mwezi Aprili mwaka juzi serikali ya muda ya Mali iliyoundwa na makanali wa jeshi ilitangza kuwa kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo itafanyika mwezi Oktoba.
Siku chache zilizopita vyama vya kidini, kitamaduni na kisiasa nchini Mali vilimtaka mkuu wa serikali ya kijeshi, Kanali Asimi Guetta, kuanzisha mashauriano kwa lengo la kutupilia mbali kipengee cha rasimu ya katiba mpya kinachosisitiza kuwa serikali ya nchi hiyo itakuwa ya kilaiki.
Vyama hivyo vilitahadharisha kwamba, iwapo hilo halitafanikiwa, vitaanzisha kampeni ya kupiga kura ya kuikataa rasimu ya katiba katika kura ya maoni itakayofanyika Juni 18.
Taarifa ilitotolewa na vyama hivyo imesema, kamati iliyopewa jukumu la kupitia rasimu ya katiba ilipaswa kuikomboa Mali kutoka kwenye “kizuizi cha itikadi iliyorithiwa kutoka kwa Ufaransa”, lakini imekosa “ujasiri”.