Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi waandamizi wa vyama vya Republican na Democratik katika bunge, wanatazamiwa kukutana Jumanne katika Ikulu mjini Washingtoin DC, huku kukiwa na mvutano kuhusu suala la kuongeza kikomo cha madeni ya taifa.
Spika wa baraza la wawakilishi, Kevin McCarthy, na Kiongozi wa wachache katika Seneti, Mitch McConnell, wataungana na kiongozi wa chama cha Democratik katika baraza la wawakilishi, Hakeem Jeffries, na Kiongozi wa wengi katika Seneti, Chuck Schumer, huku kundi hilo likijadili makataa yanayokaribia, kuhakikisha kuwa serikali inaweza kulipia matumizi ambayo yamefanyika tayari.
Warepublican wanasisitiza kupunguzwa kwa matumizi kabla ya kukubali kuongeza kiwango cha deni, wakati Rais Biden akisema bunge lina jukumu la kuhakikisha kwama serikali inalipa madeni yake, na kwamba masuala hayo mawili yanapaswa kushughulikiwa sambamba. Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen aliwaambia wabunge wiki iliyopita kwamba uwezo wa serikali kulipa madeni yake unaweza kufika mwisho mapema mwezi Juni.
Yellen alikiambia kituo cha televishen cha CNBC kwamba kulikuwa na “pengo kubwa sana” kati ya misimamo ya warepublikan na wademokrat na akaonya kwamba kutoongeza kikomo cha deni kutasababisha “janga la kiuchumi.”