Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amelishtumu jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutofanya vya kutosha kudhibiti utovu wa usalama Mashariki mwa nchi yake.
Tshisekedi ametoa kauli hiyo katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Botswana na kudai kuwa kikosi hicho kinashirikiana na waasi wa M 23 na huenda kikaondoka nchini mwake kufikia mwisho wa mwezi Juni.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Botswana, Tshisekedi alielezea wasiwasi wake kuhusu “kuishi pamoja” kati ya waasi na kikosi hicho cha Afrika Mashariki ambacho kilianza kupelekwa DRC mwishoni mwa mwaka jana.
Makundi mengi yenye silaha yanavuruga usalama Mashariki mwa DRC.
Kundi la M23, limeanzisha mashambulizi tangu lilipoibuka tena baada ya kusambaratika mwishoni mwa mwaka 2021.
Jumuia ya Afrika Mashariki yenye nchi wanachama saba iliunda kikosi cha kijeshi kukabiliana na mzozo mwezi Juni mwaka jana, huku wanajeshi wa Kenya wakipelekwa mwezi Novemba wakifuatiwa baadaye na wanajeshi wa Burundi, Uganda na Sudan Kusini.
Kauli yake inakuja siku moja baada ya mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya SADC nchini Namibia, ambako jumuiya hiyo imesema itatuma vikosi vyake Mashariki mwa DRC.
Matamshi yake pia yanakuja baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kamanda wa kikosi hicho nchini DRC Jenerali Jeff Nyagah katika kile kilichodaiwa ni kutokuwepo kwa maelewano na uongozi wa nchi hiyo ambao pia ulikosoa utendakazi wake.
Aidha mkuu huyo wa DRC alisema kuwa muda wa vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki utakapofika tamati mwishoni mwa mwezi Juni watafanya tathmini kuona iwapo kikosi hicho kitakuwa kimefanya kazi yake na baadae watafanya maamuzi kuona namna watakavyolinda nchi yao ya Kongo.