Jeshi la Polisi Tanzania limemuaga rasmi aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro, leo tarehe 10 Mei 2023 baada ya kustaafu Utumishi ndani ya Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria mwezi Machi 2023 ambapo baada ya kuagwa amekabidhiwa gari mpya (Zero KM) ambayo ataitumia katika maisha yake yote kipindi akiwa nje ya Utumishi wa Jeshi la Polisi.
Sherehe za kumuaga IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro zimefanyika katika Chuo cha
Taaluma ya Polisi Dares Salaam (DPA) kilichopo Kurasini Jijini Dar es salaam kwa gwaride maalum la kumuaga ikiwa ni utaratibu wa Jeshi la Polisi kuwaaga kwa gwaride maalum Viongozi wa Polisi waliofikia cheo cha Kamishna wa Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi.
Polisi imesema IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro amelitumika Jeshi la Polisi kwa miaka 30 tangu tarehe 19 Februari 1993 alipojiunga rasmi hadi kustaafu mwezi Machi, 2023 na ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wa 10 kuliongoza Jeshi la Polisi tangu uhuru na ameliongoza kuanzia tarehe 28 Mei 2017 hadi tarehe 20 Julai 2022 na kupata mafanikio makubwa kwenye mapambano dhidi ya uhalifu na Wahalifu ikiwemo kukomesha vitendo vya mauaji yaliyokuwa yakitokea Wilayani Kibiti na maeneo mengine pamoja na kupunguza uhalifu nchini.
Wakuu wa Jeshi la Polisi waliomtangulia ni IGP Mstaafu Elangwa Shaidi ambaye ni IGP wa kwanza tangu uhuru aliyeliongoza Jeshi La Polisi Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1970, IGP mstaafu Hamza Azizi (1970 – 1973), IGP mstaafu Samweli Pundugu (1973 – 1975), IGP Mstaafu Philemon Mgaya (1975 – 1980), IGP Mstaafu Solomon Liani (1980 – 1984), IGP Mstaafu Harun Mahundi (1984 – 1996) IGP Mstaafu Omari Mahita (1996 – 2006), IGP Mstaafu Saidi Mwema (2006 – 2013) na IGP Mstaafu Ernest Mangu (2013 – 2017).
PLAY: GWARIDE MAALUM LILIVYOINGIA KUMUAGA IGP MSTAAFU SIRRO, WAMBURA NA MNADHIMU JWTZ WAWASILI