Mashirika ya afya yanaonya kwamba homa ya ini inaweza kuua watu wengi zaidi ifikapo mwaka wa 2040 kuliko HIV, kifua kikuu, na malaria kwa pamoja ikiwa ugonjwa huo utaendelea kupuuzwa na kutofadhiliwa vya kutosha.
Shirika la afya duniani (WHO) linaripoti kila mwaka kwamba homa ya ini, inaathiri zaidi ya watu milioni 350 ulimwenguni na kuua zaidi ya watu milioni 1. Asilimia 90 ya watu wanaoambukizwa na kuuawa na ugonjwa huo ni kutoka nchi zenye pato la chini na la kati.
Licha ya tiba ya homa ya ini aina ya C na chanjo dhidi ya homa ya ini aina ya B, watetezi wa ulimwengu usio na ugonjwa huu hatari na unaoodhofisha bado hawajafikia lengo lao.
“Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika safari hii ya kutokomeza homa ya ini,” amesema Oriel Fernandez, mkurugenzi mkuu wa mpango wa homa ya ini duniani kwenye kituo cha Clinton Health Access Initiative au CHAI.
“Gharama ya jumla ya kuponya mgonjwa ilishuka kwa asilimia 96 kutoka zaidi ya dola 2,500 kwa kila mtu hadi chini ya dola 80 kwa kila mtu aliyeponywa, Oriel amesema.
Ingawa kuna aina tano tofauti za homa ya ini ya virusi (A, B, C, D, na E), homa ya ini ya muda mrefu ya B na C husababisha 95% ya magonjwa yanayohusiana na homa ya ini na vifo vya mapema.
Hepatitis D haipatikani sana na hutokea tu kwa kushirikiana na hepatitis B.
Virusi vingine (yaani hepatitis A na E) huenea kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na kusababisha maambukizi ya papo hapo na milipuko katika maeneo ya usafi duni na utupaji wa taka usiofaa.
Maambukizi ya papo hapo mara nyingi ni ya muda mfupi na kutatuliwa ndani ya wiki chache. Katika wanawake wajawazito, maambukizi ya virusi vya hepatitis E (HEV) huwa na kiwango cha juu cha vifo.
chanzo: VOAnews