Siku ya Jumatano hatimaye Iran iliwanyonga wanaume saba katika magereza mawili nje ya Tehran kwa mashtaka kuhusiana na dawa za kulevya na ubakaji, shirika la kutetea haki za binadamu limesema, na kuharakisha kile wanaharakati wanachokielezea kama msururu wa kuwanyonga watu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Wanaume watatu walinyongwa kwa mashtaka yanayohusiana na dawa za kulevya katika gereza ya Ghezal Hesar katika mji wa Karaj nje ya Teheran, shirika la haki za binadamu lenye makao yake Norway, au IHR, limesema.
Limeongeza kuwa wanaume wengine wanne walinyongwa kwa mashtaka ya ubakaji katika gereza ya Rajai Shahr, ilioko pia katika mji wa Karaj.
Tovuti ya mahakama, Mizan, ilithibitisha kunyongwa kwa watu watatu kwa mashtaka ya dawa za kulevya, ikisema washtakiwa hao walikuwa wanachama wa genge la kusambaza dawa ya kulevya aina ya cocaine. Hakuna taarifa rasmi iliyothibitisha kunyongwa kwa watu wanne kwa mashtaka ya ubakaji.
Shirika la IHR limesema Iran iliwanyonga takriban watu 64 katika siku 12 zilizopita pekee.
Siku ya Jumanne, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk alitoa wito kwa mamlaka ya Iran kukomesha hukumu ya kifo na kusitisha utekelezaji wote baada ya hukumu ya nadra ya Jumatatu ya kuwanyonga wanaume wawili kwa mashtaka ya kuukashifu Uislamu.
“Kwa wastani kufikia sasa mwaka huu, zaidi ya watu 10 wanauawa kila wiki nchini Iran, na kuifanya kuwa mmoja wa watekelezaji wa juu zaidi duniani,” alisema.
Kulingana na vikundi vya kutetea haki za binadamu, mauaji yaliongezeka nchini Iran kwa 75% mnamo 2022.