Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa leo litafanya kikao cha dharura mjini Geneva siku ya Alhamisi, kujadili mzozo unaoendelea nchini Sudan.
Kuna ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya raia, unyanyasaji wa kijinsia na uporaji wa hospitali.
Maelfu ya watu wamekimbia makazi yao na mashirika ya misaada yanasema hayawezi kufanya kazi kwa usalama.
Mataifa kadhaa ya Afrika, ikiwemo Sudan, yanaripotiwa kusitasita kuhusu mkutano huo unaofanyika, wakihofia kuwa unaweza kuhatarisha mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano.
Nchi ya Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano tangu Aprili 15, baada ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah Al-Burhan na naibu wake Mohammed Hamdan Daglo kutofautiana, mapigano ambayo yamesababisha maafa ya takriban watu 750.
Kufikia sasa mazungumzo ya kuleta mapatano hayajafanikiwa, lakini baadhi ya nchi wamefanikiwa kuwahamisha raia wao kutoka nchi hiyo kupitia nchi kavu, baharini na angani.