Balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini siku ya Alhamisi ameishutumu nchi hiyo kwa siri kuipatia silaha Russia, tuhuma ambazo zimezua majibu makali kutoka Pretoria.
Balozi Reuben Brigety aliuambia mkutano wa vyombo vya habari kuwa, Marekani inaamini kuwa silaha na risasi zilikuwa zimepakiwa kwenye meli ya mizigo ya Russia iliyotia nanga katika kambi ya jeshi la majini mjini Cape Town mwezi Desemba.
“Tuna uhakika kuwa silaha zilipakiwa kwenye meli hiyo, nasema sidanganyi, nina uhakika kuhusu usahihi wa madai hayo,” alisema Brigety kulingana na video ya matamshi hayo.
“Kuipa silaha kwa Russia kulikofanywa na Afrika Kusini… kimsingi ni jambo lisilokubalika.”
Lakini ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa ilijibu, kwa kusema kwamba “inasikitisha” kuwa Brigety “amechukua hatua ambayo haionyeshi picha nzuri”.
Matamshi hayo “yanadhoofisha hali ya mshikamano na ushirikiano” kati ya mataifa hayo mawili, msemaji wa Ramaphosa, Vincent Magwenya alisema katika taarifa yake.
Washington imeonya mara kwa mara nchi dhidi ya kutoa msaada kwa Urusi, na kuonya kwamba wale wanaofanya hivyo wanaweza kunyimwa ufikiaji wa masoko muhimu zaidi ulimwenguni.
Mapema mwaka huu, Afrika Kusini ilifanya mazoezi ya kijeshi na Russia pamoja na China, na mwezi uliopita ndege ya mizigo ya kijeshi ya Russia iliyowekewa vizuizi ilitua katika kambi ya jeshi la anga usiku wa manane kupeleka kile ambacho mamlaka ya ulinzi ilikieleza kuwa “barua ya kidiplomasia.”